HAPA KAZI TUUUUUUUUUU

Sasa mambo yamepamba moto, hii ishu ya kutumbua majipu
imefika mahala pake dahh. Juzi nilipata kazi ya kuwa
mshenga. Rafiki yangu flani ambaye mambo ya fedha kwake
si tatizo, ila tatizo ni namna ya kuzitumia fedha hizo
kaniomba niwe mshenga wake. Alikuwa anataka kupeleka
posa kwa binti mmoja ambaye ni kabila langu hivyo mimi
nilitegemewa kuwa najua mila na taratibu za kutoa posa. Basi
kama tulivyokuwa tumepangiwa na wakwe watarajiwa, juzi
saa kumi jioni tukawasili kwa wakwe watarajiwa. Tulichelewa
kama dakika tano si unajua foleni tena, hiyo ikawa nongwa ya
kwanza. Wajomba wakatuambia turudi wiki inayofuata
tukajifunze namna ya kuwahi, tukaanza kuomba msamaha na
kubembeleza, baada ya faini ya shilingi alfu ishirini
tukaruhusiwa kusikilizwa. Tulimkuta baba wa binti na
wajomba wawili wanatusubiri, tukakaribishwa kwenye viti na
kukaribishwa vinywaji. Tukaomba maji, unajua siku kama hii
ukiomba bia kabla hawajapokea barua inaweza kuwa kisa cha
kukataa kupokea barua, utasikia wanasema wakwe wenyewe
walevi, kwa hiyo ni muhimu kuwa falafala kiasi. Hatimae
tukaulizwa shida yetu. Nikasimama nikatambulisha msafara
wangu, kabla sijaanza kuongea, mjomba mmoja akaniuliza,
‘Hivi kweli we unajua mila zetu?” Nikamjibu ndio.
Akanikumbusha kuwa kwa siku hiyo ni lazima niwe naongea
huku nimepiga magoti. Mwanaume nikaomba msamaha na
kupiga magoti mbele ya baba mkwe. Kwa sauti ya unyonge
nikaeleza kuwa tumemuona binti pale kwake na tulikuwa
tunaomba kuleta barua ya kuunga ukoo. Nikaanza kusailiwa
kuhusu muoaji, hali yake ya kimaisha na kadhalika. Kwa kuwa
jamaa yangu maarufu pale mtaani, ilikuwa rahisi kuwataarifu
kuwa muoaji ni kijana mwenye uwezo wa kumtunza binti,
tayari ana mjengo wa nguvu si mbali na pale na ana magari
kadhaa mengine ya bei mbaya na kwa ujumla mtoto wao
hatapata shida maishani. Wale wazee wakatuomba tutoke nje
wajadili kitu. Dakika chache baadae tukaitwa tena ndani.
Mjomba mmoja wapo akaanza. ‘Umesema muoaji ndie
mwenye kaghorofa hapo bondeni?’ Nikajibu ndio. ‘Na huyo
muoaji si huyu mwenye lile gari jekundu lenye maspika yana
kelele akipita hapa mtaani?’ Nikatikisa kichwa kukubali maana
jamaa yangu bishoo sana ndio zake hizo. Maswali
yakaendelea, ‘Hivi anafanya kazi wapi?’. Nikawajibu
mfanyabiashara. ‘Biashara gani?’ Swali hili likawa gumu
maana hata mimi sijawahi kujua jamaa anafanya biashara
gani. Nikajibu sina uhakika. Hapo wale wazee wakanambia,
‘Rudi na barua yako. Lile ghorofa litabomolewa siku hizi hizi
maana liko eneo la bonde la mto, na kwa kuwa biashara ya
ndugu yako haijulikani atatumbuliwa jipu siku hizihizi unataka
binti yetu aanze maisha kwa kumpeleka mumewe uji
magereza? Ondokeni haraka hapa na kiposa chenu’ Daah
saa 2 · TUCHEKE KIMYA KIMYA

Comments